Friday, May 4, 2012

Basi la NBS lapata ajali mbaya-Tabora

Abiria saba wamefariki dunia na wengine 54 wamejeruhiwa vibaya, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Arusha kupasuka tairi la mbele na kisha kupinduka. Ajali hiyo iliyohusisha basi la kampuni ya NBS yenye makao yake makuu mjini Tabora, ilitokea saa 3.30 asubuhi nje kidogo ya mji wa Igunga, mkoani Tabora. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa gurudumu la mbele la upande wa kushoto kisha kupinduka. Kamanda Rutta alisema kuwa kati ya waliofariki watatu ni wanawake, watatu ni wanaume na  mtoto mmoja ambaye hata hivyo, jinsia yake haikujulikana mara moja. Aliwataja waliofariki na kutambuliwa hadi kufikia jana mchana kuwa ni Zaituni Mziray, Ernesto Iromo, Dickson Nasan na Zainabu Hamud. Kwa mujibu wa Kamanda Rutta, marehemu watatu bado hawajambuliwa majina yao kutokana na kutokuwa na vitambulisho. Alisema kuwa zoezi la kuwatambua linaendelea kufanywa chini ya uangalizi wa Polisi na kwamba majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Igunga. Kamanda Rutta alisema kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 978 ATM aina ya Scania 94, Idd Hussein Nyohi (33), alinusurika katika ajali hiyo na ni miongoni mwa majeruhi waliolazwa na kwamba analalamika kuwa na maumivu makali kifuani. Alisema majeruhi wote wanaendelea vizuri na matibabu na hakuna mwenye kuhitaji huduma ya rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi hadi sasa. Hata hivyo, Kamanda Rutta alisema bado madaktari wanaendelea kuwafanyia uchunguzi zaidi majeruhi ili kujua kama kuna madhara zaidi.

0 comments:

Post a Comment